Storm FM

Wazee Nyankumbu Geita wapatiwa msaada

13 January 2026, 12:19 pm

Miongoni mwa wazee wa Kata ya Nyankumbu waliopatiwa msaada na Kikundi cha Nyankumbu Shule Group. Picha na Mrisho Sadick

Malengo ya kikundi hicho kuendelea kurudisha kwa jamii kwa kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na wazee, watoto yatima na familia zisizojiweza.

Na Mrisho Sadick:

Wazee wanaoishi katika mazingira magumu katika Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita, wameishukuru Kikundi cha Nyankumbu Shule Group kwa kuwasaidia mahitaji ya msingi yakiwemo chakula, mavazi na mahitaji mengine muhimu ya kila siku, huku wakitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hususan wazee, yatima na watu wenye ulemavu.

Wazee hao wanaotoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Nyankumbu wamesema msaada huo umekuwa faraja kubwa kwao, hasa ikizingatiwa changamoto za maisha wanazokutana nazo ikiwemo ukosefu wa kipato na huduma muhimu za kijamii.

Viongozi wa kikundi na serikali wakiwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa kikundi hicho. Picha na Mrisho Sadick

Wakizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Kikundi hicho, viongozi wa Nyankumbu Shule Group , ambacho kinaundwa na wanafunzi waliosoma katika Shule ya Msingi Nyankumbu na chenye wanachama zaidi ya 200, wamesema kuwa lengo lao ni kuendelea kurudisha kwa jamii kwa kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na wazee, watoto yatima na familia zisizojiweza.

Baadhi ya wazee wa Kata ya Nyankumbu waliopata nafasi ya kupatiwa msaada.Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyankumbu Paschal Sukambi amekipongeza Kikundi cha Nyankumbu Shule Group kwa moyo wao wa kujitolea na kuwahimiza vijana na vikundi vingine kuiga mfano huo, akisisitiza kuwa maendeleo ya jamii yanahitaji mshikamano na ushirikiano wa pamoja nakwamba Halmashauri itaendelea kushirikiana na vikundi vya kijamii ili kuhakikisha makundi yenye uhitaji yanapata msaada stahiki na maisha yao kuboreshwa.

Sauti ya Ripoti hii na Mrisho Sadick