Storm FM
Storm FM
8 January 2026, 12:40 pm

Hatua ya kufunga cheni inalenga kudhibiti waendesha pikipiki wanaojihusisha na shughuli za usafirishaji bila kuwa na vitambulisho.
Na Kale Chongela:
Uongozi wa egesho la pikipiki la Lukilini lililopo Mtaa wa Mkoani Kata ya Kalangalala Manispaa ya Geita umeanza kutekeleza agizo la Umoja wa Bodaboda Taifa linalowataka waendesha pikipiki wote kuwa na vitambulisho vya kazi vyenye taarifa zao muhimu ikiwa ni hatua ya kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama.
Utekelezaji wa agizo hilo umeibua mvutano baada ya pikipiki ya Joseph Hamis mkazi wa Kijiji cha Bugarama Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kuzuia pikipiki yake kufungwa cheni katika egesho hilo kwa madai kuwa hana kitambulisho kinachomruhusu kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa taratibu zao.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, msimamizi wa egesho la bodaboda eneo la Lukilini Kata ya Kalangalala Bw. Siwema Saga amekiri kutokea kwa mvutano huo na kueleza kuwa hatua ya kufunga cheni inalenga kudhibiti waendesha pikipiki wanaojihusisha na shughuli za usafirishaji bila kuwa na vitambulisho halali ikiwa ni kinyume na agizo la umoja wa bodaboda Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Geita Ndugu Fred Fidel amesisitiza kuwa agizo hilo ni la lazima kwa waendesha pikipiki wote huku akiwataka wasimamizi wa maegesho kutumia njia rafiki za staha na zenye kuelimisha katika utekelezaji wa ukamataji na ufungaji cheni kwa wanaokiuka taratibu, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.