Storm FM
Storm FM
13 November 2025, 1:30 pm

Kwasasa gunia la viazi mviringo limepanda kutoka shilingi elfu sabini na tano 75,000 hadi zaidi ya laki moja 100,000
Na Mrisho Sadick:
Wafanyabiashara wa viazi mviringo katika soko la Nyankumbu mkoani Geita wameamua kupandisha bei ya bidhaa hiyo kutokana na upatikanaji wake kuwa mdogo tofauti na kipindi cha nyuma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema kwa sasa gunia la viazi mviringo limepanda kutoka shilingi elfu 75,000 hadi zaidi ya laki moja (100,000), hali ambayo imesababisha faida wanazopata kupungua kwa sababu wateja wengi hawawezi kumudu bei hizo mpya.
Wameeleza kuwa upatikanaji mdogo wa viazi unatokana na changamoto ya vurugu zilizotokea nchini Oktoba 29,2029 wakati wa uchaguzi mkuu nakufanya usafirishaji wa biadhaa hizo kukwama hali ambayo imechangia kwa kiwango kikubwa ongezeko la bei.

Kupanda kwa bei ya viazi kumeathiri pia biashara ya chipsi katika mji wa Geita, ambapo wafanyabiashara wa vyakula hivyo wamesema gharama ya malighafi imepanda kwa kiwango kikubwa, na hivyo kulazimika kuongeza bei ya sahani ya chipsi kutoka shilingi 2,500 hadi 3,000.

Wafanyabiashara hao wameomba serikali kupitia wizara husika kusaidia katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa mazao pamoja na kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji, ili kuhakikisha upatikanaji wa viazi unakuwa wa uhakika na bei zinabaki kuwa nafuu kwa wananchi.