Storm FM

Mikutano 65 ya injili yaleta mabadiliko makubwa Geita

21 October 2025, 8:23 am

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa Injili Buzanakai Nyamalimbe Geita. Picha na Kale Chongela

Lengo la huduma hiyo sasa ni kufika nje ya mkoa wa Geita ili kufikisha ujumbe wa Injili kwa Watanzania wengi zaidi.

Na Kale Chongela – Geita

Uwepo wa mikutano ya Injili katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita umeendelea kuleta matokeo chanya katika jamii ambapo wananchi wengi wameanza kuachana na matendo yasiyofaa na kurejea katika misingi ya maadili na heshima.

Akizungumza na Storm FM katika Kijiji cha Buzanaki Kata ya Nyamalimbe wilayani Geita Mkoani Geita Mchungaji Eliya George wa Kanisa la TAG Heriwenye Moyo Safi amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa kumi mwaka huu jumla ya mikutano 65 ya Injili imefanyika katika maeneo mbalimbali ya Geita na matokeo yake yameonekana wazi kupitia mabadiliko ya kitabia kwa wananchi.

Ameeleza kuwa mikutano hiyo imekuwa chanzo cha amani, upendo na mshikamano katika jamii, huku watu wengi wakirejea katika maisha ya kiroho na kujitenga na uhalifu, ulevi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Mchungaji George wa kanisa la TAG akiwa katika Kijiji cha Buzanaki akitoa Injili. Picha na Kale Chongela

Mchungaji George amesema lengo la huduma hiyo sasa ni kufika nje ya mkoa wa Geita ili kufikisha ujumbe wa Injili kwa Watanzania wengi zaidi, kwa nia ya kuijenga jamii yenye hofu ya Mungu na kuimarisha umoja.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho January Malimbagula amesema kuwa eneo lake limekuwa likitoa kipaumbele kwa watumishi wa Mungu kwa kuwapa nafasi ya kufanyia mikutano nakwamba amesema tangu kuanza kwa mikutano hiyo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kitabia, ikiwemo kupungua kwa vitendo vya uhalifu na kuongezeka kwa ushirikiano kati ya wananchi.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa Injili Buzanakai Nyamalimbe Geita. Picha na Kale Chongela

Aidha, baadhi ya waumini walioshiriki mikutano hiyo wameeleza kuwa kupitia mahubiri wanayoyapata wamepata mwanga wa kiroho na matumaini mapya katika maisha yao huku wengine wakirejea kanisani baada ya kuwa mbali kwa muda mrefu.

Mikutano ya Injili inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiroho na kijamii katika Mkoa wa Geita, ikichangia kujenga jamii yenye maadili mema, umoja na utulivu.

Ripoti ya stori hii na Kale Chongela