Storm FM

Chama Cha Makini chatua kwa Hayati Magufuli, chaonya maandamano

17 October 2025, 10:01 pm

Viongozi wa Chama Cha Makini wakiwa nyumbani kwa Hayati Dkt Magufuli wilayani Chato. Picha na Mrisho Sadick

Onyo kwa baadhi ya watu au makundi yanayopanga kufanya maandamano au kuchochea machafuko kabla au baada ya uchaguzi

Na Mrisho Sadick – Geita

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Makini Coaster Kibonde ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 akisisitiza kuwa kushiriki katika uchaguzi ni wajibu wa kikatiba na haki ya kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura.

Akizungumza katika wilaya ya Chato mkoani Geita baada ya kutembelea na kuweka maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli Kibonde ameeleza kuwa kunapotokea uchaguzi ni muhimu kwa kila raia kutekeleza haki yake ili kuchangia katika mchakato wa kidemokrasia na kuamua hatma ya taifa.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Makini Coaster Kibonde akizungumza baada ya kuzuru kaburi la JPM. Picha na Mrisho Sadick

Katika hatua nyingine mgombea huyo amezungumzia hali ya amani kuelekea uchaguzi akitoa onyo kwa baadhi ya watu au makundi yanayopanga kufanya maandamano au kuchochea machafuko kabla au baada ya uchaguzi kwakuwa maandamano yasiyo halali yanaweza kuhatarisha utulivu wa taifa.

Aidha ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa mazingira ya uchaguzi yanabaki kuwa salama, huru na ya haki ili kila mwananchi aweze kutekeleza haki yake bila woga wala hofu.

Nyumba ya milele ya Hayati Dkt Magufuli wilayani Chato Mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Chama cha Makini kinatarajiwa kuendelea na kampeni zake katika mkoa wa Geita kwa lengo la kuwasilisha ilani ya chama na kuwashawishi wananchi kuhusu ajenda zake.

Sauti ya Ripoti ya stori hii