Storm FM

Geita Gold yawasha taa nyenkundu, Barberian kala tatu kavu

11 October 2025, 9:59 pm

Kocha Mkuu wa Geita Gold Zuberi Katwila akizungumza baada ya mchezo kumalizika. Picha Mrisho Sadick

Ushindi huo unaifanya Geita Gold kuanza msimu mpya wa Championship kwa alama tatu muhimu, huku ikionesha dhamira ya wazi ya kurejea katika Ligi Kuu

Na Mrisho Sadick:

Timu ya Geita Gold FC imeanza kwa kishindo safari yake ya kutafuta kurejea Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Barberian FC katika mchezo wa kwanza wa Nyumbani wa Championship uliofanyika kwenye Uwanja wa Nyankumbu Girls Manispaa ya Geita.

Katika mchezo huo Geita Gold imeonesha kandanda safi na nidhamu ya hali ya juu tangu filimbi ya kwanza, mabao ya Geita Gold yamefungwa kupitia kwa Omary Omary ambae amefunga mawili na Mauld Shabani bao moja.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo Kocha Mkuu wa Geita Gold Zuberi Katwila, amesema ameridhishwa na jinsi wachezaji wake walivyotekeleza maelekezo yake hasa kwenye nidhamu ya uchezaji na umaliziaji huku Kocha wa Barberian FC Morisi Kamongo amekiri timu yake kufanya makosa kadhaa lakini akaahidi kuyafanyia kazi kabla ya mchezo unaofuata.

Sauti ya makocha wa timu zote mbili
Kocha wa Barberian FC Morisi Kamongo akizungumza baada ya kupoteza mchezo wa kwanza.Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake msemaji wa Geita Gold FC Samweli Dida amezungumzia mwanzo mzuri wa msimu mpya wa Championship akieleza kuwa kikosi cha timu hiyo kiko katika kiwango kizuri na kimejiandaa kupanda ligi kuu nakwamba nguvu kubwa ya Geita Gold ni sapoti kubwa ya mashabiki walioko uwanjani amewapongeza mashabiki ambao wamejitokeza kwa wingi huku akiwaahidi kuwa timu hiyo itafanya vizuri msimu huu.

Msemaji wa Geita Gold Samwel Dida akizungumza baada ya ushindi mnono. Picha na Mrisho Sadick
Sauti ya msemaji Geita Gold FC

Ushindi huo unaifanya Geita Gold kuanza msimu mpya wa Championship kwa alama tatu muhimu, huku ikionesha dhamira ya wazi ya kupanda daraja na kurejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.