Storm FM

Idadi ya watalii yazidi kuongezeka kisiwa cha Rubondo

8 October 2025, 6:07 pm

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo Dkt. Imani Kikoti akizungumzia hifadhi hiyo. Picha na Mrisho Sadick

Hifadhi hiyo inajivunia kuwa na fukwe za mazalia ya samaki zenye urefu wa zaidi ya kilometa 150 hali ambayo inakifanya kisiwa hicho kuwa za kipekee

Na Mrisho Sadick:

Idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo kilichopo wilayani Chato mkoani Geita imeendelea kuongezeka kutokana na jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha miundombinu na kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko katika hifadhi hiyo.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo Dkt. Imani Kikoti amesema kwa sasa hifadhi hiyo inapokea zaidi ya watalii 5,000 kwa mwaka kutoka ndani na nje ya nchi nakwamba ongezeko hilo limechangiwa na maboresho makubwa ya barabara, usafiri wa majini, na huduma za malazi kwa watalii.

Dkt. Kikoti ameongeza kuwa Hifadhi ya Rubondo ni miongoni mwa maeneo ya kipekee duniani kutokana na kuwa hifadhi ambayo ina maajabu ya kipekee , hifadhi hiyo inajivunia kuwa na fukwe za mazalia ya samaki zenye urefu wa zaidi ya kilometa 150, misitu minene, pamoja na wanyamapori mbalimbali wakiwemo sokwe, viboko, tembo, nyani, mamba.

Moja ya picha iliyopigwa kwa juu kutoka katika kisiwa cha Rubondo. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Kitengo cha Ulinzi Agricola Roman amesema TANAPA imeimarisha doria katika eneo la hifadhi kwa kushirikiana na wananchi wanaoishi kandokando ya Ziwa Victoria ili kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu na kuhakikisha usalama wa watalii unaendelea kuimarika.

Baadhi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo wamesema wamevutiwa na mandhari ya asili ya hifadhi hiyo, ikiwemo fukwe safi, utulivu wa mazingira na huduma bora zinazotolewa na watumishi wa TANAPA,wameeleza kuwa Rubondo ni eneo linalofaa kwa utalii wa mapumziko na tafiti za kisayansi.

Bango la hifadhi ya taifa kisiwa cha Rubondo likiwa katika jengo la hifadhi hiyo. Picha na Mrisho Sadick

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo ni miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii vilivyoko katika Kanda ya Ziwa, ikijumuishwa na hifadhi nyingine kama Serengeti, Burigi–Chato, Ibanda–Kyerwa na Biharamulo. Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara na usafiri wa anga ili kuunganisha vivutio hivyo na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea maeneo hayo.

Kwa sasa, TANAPA imeweka mkakati wa kuongeza kampeni za utalii wa ndani, ili kuwahamasisha wananchi zaidi kutembelea hifadhi za taifa, huku Hifadhi ya Rubondo ikitarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayovutia wageni wengi zaidi katika miaka michache ijayo.

Ripoti kamili ya stori hii na Mrisho Sadick