Storm FM
Storm FM
8 October 2025, 5:30 pm

Kwa sasa hifadhi hiyo inaendelea kuboresha huduma za utalii, ikiwa ni pamoja na usafiri wa majini, malazi ya kisasa na shughuli za uhamasishaji wa utalii wa ndani.
Na Mrisho Sadick:
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo iliyopo wilayani Chato mkoani Geita ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa nyumba za kifahari zitakazotumika na watu mashuhuri pamoja na watalii wa ndani na kimataifa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wa kuhakikisha kisiwa hicho kinakuwa moja ya kivutio bora na chakipekee barani Afrika.
Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza wa Hifadhi hiyo Bruno Felix Assey amesema kuwa mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza ubora wa huduma na kuvutia watalii wa hadhi ya juu kutoka ndani na nje ya nchi.

Assey amebainisha kuwa Rubondo ni hifadhi ya kipekee yenye mchanganyiko wa vivutio vya ziwani misitu minene, wanyamapori wa aina mbalimbali pamoja na ndege adimu ambao hawaonekani maeneo mengine nchini na sehemu za afrika.
Kupitia uwekezaji huo hifadhi inatarajiwa kuongeza mapato ya utalii na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaoishi kandokando ya hifadhi, TANAPA imekuwa ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati yake na jamii zinazozunguka hifadhi jambo linalosaidia katika kupunguza vitendo vya ujangili na uharibifu wa mazingira.
Maafisa wa hifadhi hiyo Amina Said na Zacharia Kimambo wamesema kuwa Rubondo inabaki kuwa moja ya maeneo machache yenye utulivu na mazingira asilia yaliyohifadhiwa vizuri,ikijivunia uwepo wa wanyama kama tembo, sokwe, viboko, twiga na wengine, pamoja na takribani aina 200 za ndege wa asili na wa kuhama.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TANAPA Catherine Mbena ameeleza kuwa ushirikiano mzuri kati ya wananchi na mamlaka ya hifadhi umekuwa chachu kubwa ya mafanikio hayo nakwamba jamii zinazozunguka hifadhi zimekuwa mfano wa kuigwa kwa namna zinavyoshiriki katika kulinda urithi wa taifa.
Kwa sasa hifadhi hiyo inaendelea kuboresha huduma za utalii, ikiwa ni pamoja na usafiri wa majini, malazi ya kisasa na shughuli za uhamasishaji wa utalii wa ndani, utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuhakikisha Rubondo inapata hadhi ya kimataifa na kuwa sehemu muhimu katika kukuza sekta ya utalii inayochangia pato la taifa.