Storm FM
Storm FM
6 October 2025, 1:58 pm

Vijana hao wameeleza kuwa hawatashiriki katika vurugu, maandamano yasiyo ya lazima au propaganda za kisiasa.
Na Mrisho Sadick:
Vijana kutoka makundi mbalimbali ikiwemo vyuo na shule za sekondari katika Manispaa ya Geita Mkoani Geita wamesema wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Vijana hao wamebainisha hayo kwenye Mdahalo kuhusu umuhimu wa vijana kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, ulioandaliwa na Shirika la NELICO kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana.

Mdahalo huo umebeba ajenda muhimu ambapo baadhi ya vijana hao wamesema kupitia elimu waliyoipata kwenye mdahalo huo, wameelewa kuwa kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kila kijana anayejali mustakabali wa taifa.
Sambamba na hayo, vijana hao wameeleza kuwa hawatashiriki katika vurugu, maandamano yasiyo ya lazima au propaganda za kisiasa, bali watatumia siku ya Oktoba 29 kutekeleza wajibu wao wa kikatiba kwa amani na utulivu.

Mkurugenzi wa Shirika la NELICO, Paulina Majogoro, amewataka vijana hao kutumia haki yao ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaojali maslahi ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla nakukataa kutumika vibaya ikiwemo kufanya maandamano.