Storm FM

Viongozi wa dini Geita wakemea viashiria uvunjifu wa amani

6 October 2025, 12:11 pm

Viongozi wa dini Geita wakiwa kwenye mdahalo wa umuhimu wa amani. Picha na Mrisho Sadick

Viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kuhimiza amani kwa waumini wao kwani ni wadau muhimu katika kulinda tunu ya taifa.

Na Mrisho Sadick:

Viongozi wa dini Mkoani Geita wamekemea vikali viashiria vya uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu, wakiwataka Watanzania kuwapuuza watu wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza chuki na maneno ya uchochezi.

Mdahalo wa kujadili umuhimu wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu umeandaliwa na Shirika la NELICO lenye makao makuu yake Geita, likiwashirikisha viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali kwa kuwa viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kuhimiza amani kwa waumini wao kwani ni wadau muhimu katika kulinda tunu ya taifa.

Viongozi wa dini Geita wakiwa kwenye mdahalo wa umuhimu wa amani. Picha na Mrisho Sadick

Baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wamesema ni muhimu Watanzania wakatambua thamani ya amani kwa sababu nchi nyingi zenye machafuko zimeanza kwa maneno madogo ya uchochezi, ametolea mfano wa machafuko yanayoendelea nchini Congo DR ambapo wananchi wengi wamelazimika kukimbia makazi yao na huduma muhimu za kibinadamu kama afya na elimu zimesimama kutokana na vita.

Sauti ya viongozi wa dini
Mkurungezi wa NELICO kulia akiwa na mwezeshaji wa mdahalo kushoto. Picha na Mrisho Sadick

Katika hatua nyingine, viongozi hao wa dini wamewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawakanya vijana wao wanaodhani amani ni kitu cha kuchezea wakisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa walinzi wa amani huku wakiwaonya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kueneza chuki na tofauti za kisiasa, jambo ambalo linaweza kuhatarisha umoja wa taifa hivyo jamii inapaswa kuwa makini.

Sauti ya viongozi ya dini

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la NELICO Paulina Alex Majogoro amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kampeni za kuhimiza amani na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu ujao nakwamba viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii kupitia nyumba za ibada na kuwahimiza waumini kutanguliza amani badala ya hasira au chuki wakati wa mchakato wa kisiasa.

Sauti ya Mkurugenzi wa NELCO