Storm FM
Storm FM
24 September 2025, 10:20 am

Changamoto kubwa kwa wananchi wa Nyankumbu ni usalama na mazingira bora ya kufanyia biashara, hivyo utekelezaji wa ahadi hizo utakuwa mkombozi
Na Mrisho Sadick:
Mgombea Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita mkoani Geita, Paschal Sukambi ameahidi kusimamia mradi wa kuweka taa katika masoko ya jioni pamoja na ujenzi wa kituo cha Polisi kitakachotoa huduma saa 24.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika Mtaa wa Mkolani mjini Geita, Sukambi amesema changamoto kubwa kwa wananchi wa Nyankumbu ni usalama na mazingira bora ya kufanyia biashara, hivyo utekelezaji wa ahadi hizo utakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla nakwamba hatua hiyo itaondoa hofu ya vitendo vya kihalifu na itasaidia kukuza uchumi wa kaya kupitia biashara zinazofanyika wakati wa jioni.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Geita Gabriel Nyasilu amewataka wakazi wa Kata hiyo kuendelea kuiamini CCM kwa kuwa chama hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku akitaja mafanikio yaliyopatikana katika sekta za afya, elimu, maji safi na salama pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, akibainisha kuwa yote hayo ni matunda ya uongozi thabiti wa CCM.

Nyasilu ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umekuwa ukigusa maisha ya wananchi moja kwa moja ambapo maboresho ya sekta ya afya yameongeza upatikanaji wa huduma za matibabu, sekta ya elimu imewapa wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia, na huduma za maji safi zimepunguza adha kubwa kwa akina mama na watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.