Storm FM
Storm FM
19 September 2025, 2:08 pm

Mamlaka hiyo itaendelea kuwa karibu na wafanyabiashara wadogo kupitia ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi.
Na Mrisho Sadick:
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita imezindua rasmi dawati maalumu la uwezeshaji biashara kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara wa makundi yote katika mkoa huo, hususan wale wa sekta binafsi ili kukuza biashara zao nakuwafanya kulipa kodi kwa hiari.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Mohammed Gombati amesema dawati hilo litakuwa chachu ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara bila kujali ukubwa wa biashara zao huku akisisitiza kuwa litawasaidia wafanyabiashara hao kulipa kodi kwa hiari na kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Awali akitoa taarifa za kuanzishwa kwa dawati hilo Meneja wa TRA Mkoa wa Geita amebainisha kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuwa karibu na wafanyabiashara wadogo kupitia ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki kwenye hafla hiyo wamesema kuanzishwa kwa dawati hilo kutawarahisishia upatikanaji wa msaada wa kibiashara na kuongeza tija kwenye biashara zao.

Sambamba na uzinduzi huo Meneja wa TRA mkoa wa Geita amesema mamlaka hiyo imevuka lengo la makusanyo kutoka bilioni 61.7 waliopangiwa, nakukusanya bilioni 69.2 kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambayo ni sawa na asilimia 113% .