Storm FM

Jeshi la zimamoto na uokoaji Geita laipongeza Storm FM

19 September 2025, 1:49 pm

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushoto akimkabidhi meneja wa Storm FM hati ya pongezi. Picha na Mrisho Sadick

Dhamira ya Storm FM ni kuendelea kuwa chombo madhubuti cha mawasiliano kwa jamii kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi elimu ya kujikinga na majanga.

Na Mrisho Sadick:

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita leo Septemba 18, 2025, limekabidhi hati ya pongezi kwa Storm FM kutokana na mchango mkubwa wa redio hiyo katika kuelimisha na kuhabarisha wananchi kuhusu masuala ya usalama na uokoaji.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Storm FM ambapo Kamanda wa Jeshi hilo Mkoani Geita Mrakibu Mwandamizi Hamis Shabani Dawa ameeleza kuwa hati hiyo imetolewa kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania kama sehemu ya kutambua kazi nzuri inayofanywa na Storm FM kwa kushirikiana na taasisi za serikali katika kufikisha elimu kwa umma.

Jeshi hilo limeeleza kuwa limejipanga vyema kukabiliana na majanga yoyote hasa katika kipindi hiki cha mwenendo wa kampeni za kisiasa, mikakati ya dharura imewekwa tayari ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mafunzo ya mara kwa mara kwa wanajamii.

Kwa upande wake Meneja wa Storm FM Obadia Mashamba amesema kuwa dhamira yao ni kuendelea kuwa chombo madhubuti cha mawasiliano kwa jamii kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi elimu ya kujikinga na majanga, pamoja na burudani yenye maadili kwakuwa redio hiyo imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na vyombo vya usalama na taasisi nyingine za serikali katika kuwaelimisha wananchi juu ya tahadhari na hatua za kuchukua wakati wa majanga.

Storm FM pia imedhamiria kuimarisha zaidi vipindi vinavyolenga usalama wa jamii na itaendelea kushirikiana na Jeshi la Zimamoto kwa karibu, ili kuhakikisha jamii ya Geita inakuwa salama na yenye uelewa wa kutosha kuhusu majanga mbalimbali.

Ripoti kamili na Kale Chongela