Storm FM

Utumikishaji punda migodini Geita uzingatie haki za wanyama

15 September 2025, 9:28 am

Punda wakiwa wamebeba mizigo ya mawe ya dhahabu katika mgodi wa Mgusu Miners Geita. Picha na Mrisho Sadick

Serikali, wamiliki na wadau kushirikiana ili kuhakikisha wanyamakazi punda wanathaminiwa na kutunzwa kwakuwa wanategemewa kiuchumi.

Na Mrisho Sadick:

Jamii mkoani Geita imetakiwa kuthamini na kulinda wanyamakazi punda ambao wamekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa baadhi ya wananchi wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika migodi ya wachimbaji wadogo Mkoani humo.

Licha ya Wanyama hao kuwa chanzo cha kipato lakini wanakutana na masaibu makubwa kila siku wakiwa wamesheheni mizigo mizito kutoka milimani mara nyingi bila chakula cha kutosha, maji safi au mapumziko hali ambayo inasababisha wengi wao kupata majeraha makubwa nakuishia kufa.

Wataalamu kutoka ASPA na Serikali wakifanya uchunguzi kwa wanyamakazi punda. Picha na Mrisho Sadick

Shirika la ASPA linalofadhiliwa na Brooke East Africa likiwa katika Mgodi wa Mgusu Miners Kata ya Mgusu Manispaa ya Geita limeendelea kutoa elimu na kampeni za kuhamasisha jamii kutambua haki za punda huku Mkurugenzi wa ASPA Dkt Livingston Masija amehimiza serikali, wamiliki na wadau kushirikiana ili kuhakikisha wanyama hawa wanaothaminiwa na kutegemewa kiuchumi wanatunzwa.

Sauti ya Mkurugenzi ASPA
Mkurugenzi wa ASPA Livingston Masija akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Mrisho Sadick

Daktari wa mifugo wa Manispaa ya Geita Jasson Mutayabarwa amesema Manispaa hiyo inakadiriwa kuwa na punda zaidi ya 820 na idadi kubwa ipo katika Kata ya Mgusu huku akisema changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu kwa wamiliki wa punda kuhusu haki za wanyama nakwamba ujio wa shirika la ASPA imeanza kubadili mtazamo wa jamii juu ya wanyama hao. 

Sauti ya Daktari wa mifugo

Afisa maendeleo wa Kata ya Mgusu Dorosela Bawayo anatambua mchango wa punda katika kuongeza kipato cha wananchi, lakini wanatambua pia kwamba faida hiyo imeambatana na mateso makubwa ya wanyama hao huku mjumbe wa bodi ya ushirika wa Mgusu Miners Erick Joseph amesema kutokana na elimu ambayo wanaipata kutoka shirika la ASPA wameendelea kuzingatia haki za mnyamakazi punda.

Sauti za viongozi Mgusu