Storm FM
Storm FM
15 September 2025, 8:25 am

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka wazi mikakati ya kuhakikisha maendeleo yanashuka hadi ngazi za chini.
Na Mrisho Sadick:
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi kampeni katika Jimbo jipya la Katoro Mkoani Geita kwa msisitizo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi hususan miundombinu ya barabara na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo Septemba 14,2025 baadhi ya wakazi wa mji wa Katoro Maua Hussein na Edson Chinyeleche wameeleza kuwa wako tayari kuwachagua madiwani ,Mbunge na Rais wa CCM katika uchaguzi mkuu, lakini wakaiomba serikali kupitia viongozi hao kuhakikisha barabara za mitaa zinaratibiwa na kurekebishwa.

Mgombea udiwani wa Kata ya Ludete Jumanne Misungwi amesema ilani ya chama hicho imeweka wazi mikakati ya kuhakikisha maendeleo yanashuka hadi ngazi za chini na kwamba changamoto zilizobainishwa na wananchi zitakuwa sehemu ya utekelezaji wa ahadi za viongozi wa CCM katika jimbo hilo.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Katoro, Mhandisi Kija Limbu Ntemi, amebainisha kuwa kipaumbele chake kikubwa kitakuwa kuhakikisha jimbo hilo linapata Halmashauri mpya hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo miundombinu ya barabara, elimu, afya na maji safi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila amewahakikishia wananchi kuwa chama hicho kimejipanga kuendeleza kasi ya maendeleo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa ilani ya awamu iliyopita umefanyika kwa asilimia 100, hivyo wananchi wa Katoro wasiwe na shaka na dhamira ya CCM katika kutatua changamoto walizonazo.