Storm FM
Storm FM
12 September 2025, 5:28 am

“Kazi kubwa iliyopo kwa sasa ni kutafuta ushindi wa chama chetu na sio kuendelea kuvunja nguvu katika masuala yasiyo leta tija ndani ya chama” – Mwenyekiti Nyamaigoro
Na: Ester Mabula
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya CCM wilaya ya Geita Robert Nyamaigoro ametoa onyo kali kwa viongozi wa Jumuiya hiyo wanaoendeleza siasa za makundi ndani ya chama na kushindwa kushirikiana na wagombea waliopitishwa rasmi na chama.
Akizungumza Septemba 11, 2025 katika mkutano wa ndani uliofanyika katika Ukumbi wa CCM wilaya ya Geita Bw. Nyamaigoro amesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kata ndani ya Jumuiya hiyo ambao wamekuwa wakijihusisha na siasa za ubaguzi na kujaribu kuwatenga wagombea waliopitishwa na chama kwa sababu ya tofauti za makundi, jambo ambalo linahatarisha mshikamano na umoja ndani yaJumuiya hiyo.

Ameongeza kuwa kwa sasa ni kipindi cha Kampeni hivyo ni vyema kuelekeza nguvu katika kutafuta ushindi wa Chama hicho kwa wananchi na kwamba mchakato wa kutafuta wagombea ulihusisha hatua zote muhimu.
Katika hatua nyingine amesema Jumuiya hiyo ni nguzo muhimu ndani ya CCM na hivyo inapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kukuza demokrasia ya kweli, mshikamano na kujenga mazingira ya usawa kwa wagombea wote waliopitishwa kwa mujibu wa taratibu za chama.
