Storm FM
Storm FM
5 September 2025, 11:32 am

“Matukio ya vibaka na wezi kuiba katika mtaa huu yamekithiri hatuna amani, serikali iwashughulikie watu watakaobainika ili iwe fundisho” – Mwananchi
Na: Amon Mwakalobo
Watu wasiofahamika wanaosadikika kuwa ni wezi wamebomoa kibanda cha biashara (duka) cha Bw. Shemu Masato katika mtaa wa Msalala road, halmashauri ya manispaa ya Geita na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo sukari na mafuta ya kupikia vyenye thamani ya shilingi laki nne.
Kwa mujibu wa mama mwenye nyumba Ester Mashiri alipopanga mfanyabiashara huyo na mfanyabiashara mwenyewe wanasimulia kusikitishwa na tukio hilo ambalo lilitokea majira ya saa kumi za Alfajiri ya Septemba 04, 2025.
Mmoja wa majirani wa nyumba hiyo ambaye Jenipher Justine amesema alisikia usiku mlango ukifunguliwa kwa kelele akapuuzia akifikiri ni majirani wanapigana.
Mama mwingine mpangaji wa nyumba hiyo ambaye ni Mtaalamu wa tiba asili Bi. Maisala Shaban amesema matukio ya wizi mtaani hapo yamezidi kwani wiki iliyopita tuu walivunja mlango wa chumba chake na kutaka kumuibia dawa zake za asili lakini hawakufanikiwa.
Mlinzi wa eneo hilo akihojiwa na viongozi wa mtaa huo amesema aliacha lindo saa kumi za usiku pakiwa salama huku akiwa amefunga kamba na kwenda kulala.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bw. Sostenes Kalist amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuwashauri wafanyabiashara kuhakikisha wanakuwa na walinzi wa kampuni na si mlinzi mmoja mmoja ambaye anapata wakati mgumu kulinda peke yake eneo kubwa.