Storm FM

Serikali yatoa hekta 5,000 za hifadhi kwa wananchi Bukombe

30 August 2025, 6:00 pm

Mkuu wa mkoa wa Geita akizungumza na wakazi wa Idosero wilayani Bukombe. Picha na Mrisho Sadick

Hakuna wananchi wenye uhaba wa maeneo na makazi katika kitongoji cha Idosero baada ya serikali kutoa hekta zaidi ya 5,000.

Na Mrisho Sadick:

Serikali imetenga zaidi ya hekta 5,600 kutoka maeneo ya hifadhi na kuwagawia wananchi wa Kitongoji cha Idosero Kata ya Busonzo wilayani Bukombe Mkoani Geita ili zitumike kwa makazi, kilimo na ufugaji hatua inayolenga kupunguza migogoro baina ya wananchi na TFS.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela akizungumza na wananchi  hao leo Agosti 30,2025 amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu, ambapo serikali imeona umuhimu wa kutoa suluhu ya kudumu bila kuathiri hifadhi zilizopo.

Mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskas Muragili akiwa kwenye mkutano huo amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa hakuna wananchi wenye uhaba wa maeneo na makazi katika eneo hilo baada ya serikali kutoa hekta hizo zaidi ya 5,000 nakwamba kama kuna wananchi wanataka maeneo mapya tofauti na yaliyotolewa na serikali suala hilo halitambui.

Wakazi wa Idosero wakiwa katika mkutano wa hadhara kijijini humo. Picha na Mrisho Sadick

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Silayo Mhifadhi mwandamizi Juma Mseti amewapongeza wananchi kwa ushirikiano ambao wanaendelea kuuonesha kwenye mchakato huo na akawasihi kuendelea kuzingatia sheria na taratibu za uhifadhi nakwamba hatua hii ya serikali inatajwa kuwa sehemu ya mpango wa kupunguza changamoto za mgongano kati ya wananchi na hifadhi.

Mhifadhi mkuu shamba la miti la Silayo akizungumzia suala la serikali kutoa ardhi kwa wananchi. Picha na Mrisho Sadick

Katika mkutano huo wa hadhara baadhi ya wananchi wamedai kutoridhika na eneo lililotengwa kwa ajili yao huku serikali ikisisitiza kuwa wananchi watakaopenda kuendelea kutumia maeneo yaliyotengwa wanapaswa kuendelea na utaratibu wa kugawiwa na wale wanaohitaji maeneo mapya wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa kufuata taratibu.

Ripoti na Mrisho Sadick