Storm FM
Storm FM
27 August 2025, 4:45 pm

Uchumi wa wananchi wa Nyawilimilwa unategemea kilimo hivyo mikakati madhubuti inatakiwa kuwawezesha wananchi.
Na Mrisho Sadick:
Wakulima wa mazao ya mpunga, mihogo na mahindi katika Kijiji cha Nyawilimilwa wilaya ya Geita Mkoani Geita wamedai kukabiliwa na changamoto za kupunjwa na wanunuzi wanaowafuata mashambani pamoja na ukosefu wa pembejeo za kilimo hali ambayo wamesema inawafanya washindwe kunufaika na jasho lao.
Wakizungumza na Storm FM Juu ya changamoto hizo wakulima hao wamemtaka mgombea wa Udiwani wa Kata ya Nyawilimilwa kuhakikisha anazipa kipaumbele iwapo atachaguliwa kuwa Diwani kwa kuwa kilimo ndicho tegemeo kubwa la maisha yao ya kila siku.

Akizungumza baada ya kurudisha fomu za kugombea Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kijijini humo, Ashibel Njegene amesema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa kuhakikisha wakulima wanapata masoko yenye uhakika na pembejeo kwa bei nafuu.

Njegene alisisitiza kuwa uchumi wa wananchi wa Nyawilimilwa unategemea kilimo, hivyo kama ataaminiwa na wananchi na kuchaguliwa kuwa Diwani, atahakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi ili kuinua kipato cha wakulima na kuboresha maisha ya wananchi wa Kata hiyo.