Storm FM

Bodaboda Geita wafunguka serikali kuwaondolea kodi

26 August 2025, 4:45 pm

Waendesha bodaboda na wajasiriamali wakiwa kwenye semina ya elimu kwa mlipa kodi Geita. Picha na Edga Rwenduru

Msamaha wa kodi kwa waendesha au wamiliki pikipiki zinazotumiwa kibiashara maarufu kama bodaboda ambapo awali walikua wakilipa shilingi 65,000 kwa mwaka kwasasa hawalipi chochote.

Na Edga Rwenduru:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita imesema mabadiliko ya sheria za kodi yaliyopitishwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yamekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, hususan waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na pikipiki za miguu mitatu.

Akizungumza katika semina ya elimu kwa mlipakodi katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Geita Mkoani Geita Afisa Mkuu wa Kodi kupitia kitengo cha elimu kwa mlipa kodi TRA mkoani Geita Jastine Katiti amesema mabadiliko hayo yamelenga kupunguza kodi ambazo kwa muda mrefu zilikuwa mzigo kwa wajasiriamali wadogo na vijana wanaojihusisha na shughuli za usafirishaji.

Afisa mkuu wa kodi TRA Mkoa wa Geita akizungumzia juu ya serikali kuondoa kodi mbalimbali. Picha na Edga Rwenduru

Miongoni mwa mabadiliko hayo ya sheria ya fedha ya mwaka 2025 katika vyombo vya moto kwa kutoa msamaha wa kodi kwa waendesha au wamiliki pikipiki zinazotumiwa kibiashara maarufu kama bodaboda ambapo awali walikua wakilipa shilingi 65,000 kwa mwaka pia, sheria imepunguza kodi kwa wamiliki wa Guta kutoka Shilingi 250,000 mpaka Shilingi 120,000 kwa mwaka. 

Akizungumza niaba ya waendesha Bodaboda Mkoa wa Geita mwenyekiti wa umoja huo Fidel ameanza kwa kuipongeza serikali kwa kuwaondolea kodi hiyo ya shilingi 65,000 kwani ilikuwa kikwazo kikubwa kwao kutokana na wengi wao kukumbana na changamoto kwenye kazi hiyo.

Mwenyekiti wa umoja wa waendesha bajaji mkoa wa Geita akizungumzia kuondolewa kwa kodi ya mwaka. Picha na Edga Rwenduru