Storm FM
Storm FM
21 August 2025, 2:58 pm

Oparesheni hiyo ni endelevu na inalenga kulinda usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara Na Kale Chongela.
Na Kale Chongela:
Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani mkoani Geita limesema halitawafumbia macho madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani ikiwemo kuzidisha abiria na mwendo kasi, kwani vitendo hivyo vimesababisha ajali nyingi na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kikosi Cha usalama Barabarani Mkoa wa Geita Mrakibu wa Polisi Jacobo kufuatia oparesheni mbalimbali zinazoendelea katika wilaya zote za Mkoa wa Geita ambapo tayari baadhi ya madereva bajaji wamekamatwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo kuzidisha abiria na kuendesha bila kufuata alama za usalama barabarani.
Kwa upande wake Afisa Leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji Ardhini (LATRA) mkoani Geita, Bw. Kenani Katindasa, amesema oparesheni hiyo ni endelevu na inalenga kulinda usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara nakwamba wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha madereva wanaoendesha vyombo vya moto bila leseni au kwa kukiuka taratibu wanachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kutozwa faini na kufikishwa mahakamani.

Bw Katindasa amewataka wananchi kuacha kushawishika kupanda vyombo vya usafiri vinavyovunja sheria kwa sababu wanaweka maisha yao hatarini, huku akibainisha kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya tabia za baadhi ya madereva kuendesha kiholela, jambo linalosababisha ajali na ulemavu.
Kwa upande wao baadhi ya madereva wa bajaji waliokamatwa kwa makosa ya kuzidisha abiria na kutokuwa na nyaraka muhimu za usafirishaji wamesema wamekuwa wakilazimika kufanya hivyo kutokana na changamoto za kiuchumi na ugumu wa maisha hata hivyo wameahidi kubadilika na kufuata sheria za usalama barabarani baada ya kupata elimu kutoka kwa Jeshi la Polisi na LATRA.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi wote kushirikiana kwa kutoa taarifa za madereva wanaoendesha kihatarishi, huku likisisitiza kuwa oparesheni hiyo itaendelea katika maeneo yote ya Mkoa wa Geita kwa lengo la kupunguza ajali na kulinda maisha ya wananchi.