Storm FM
Storm FM
17 August 2025, 8:02 pm

Wamekabidhiwa ofisi hiyo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Yefred Myenzi kwa ajili ya kuanza kuitumia rasmi katika shughuli zao.
Na Kale Chongela:
Umoja wa Madereva Bodaboda Mkoa wa Geita (UMABOGE) wameipongeza serikali kwa kuwajengea ofisi mpya iliyopo katika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan (zamani EPZA) katika mtaa wa Bombambili, manispaa ya Geita.
Katibu wa umoja huo, Bw Fred Mgeta amesema kuwa wamekabidhiwa ofisi hiyo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita nakwamba ni hatua kubwa kwa kuwa sasa wanayo ofisi rasmi yenye ukumbi wa mikutano na miundombinu muhimu kwa ajili ya shuguli zao za kila siku.

Aidha, Bw. Mgeta amebainisha kuwa uwepo wa ofisi hiyo utarahisisha utendaji kazi wa umoja huo, ikiwemo kuratibu shughuli zao, kupanga mikakati ya maendeleo ya vijana madereva bodaboda, na pia kusaidia katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa urahisi zaidi.

Baadhi ya maafisa usafirishaji na madereva kwa nyakati tofauti wameshukuru hatua hiyo, wakieleza kuwa imewaondolea mzigo wa michango ya mara kwa mara waliyokuwa wakitoa ili kulipia ofisi za kupanga, na sasa fedha hizo zitatumika katika shughuli nyingine za kijamii na maendeleo.