Storm FM
Storm FM
16 August 2025, 8:15 pm

Watahiniwa 6,331 kati yao wavulana wakiwa 3,248 na wasichana 3,083 sawa na asilimia 4,17 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.
Na Mrisho Sadick:
Kamati ya Maafisa Elimu kutoka mikoa sita ya kanda ya ziwa imetangaza matokeo ya mtihani wa utamilifu (MOCK) wa kidato cha nne mwaka 2025 ambapo Mkoa wa Mwanza umeibuka kinara kwa ufaulu wa asilimia 94.11.
Matokeo hayo yametangazwa katika shule ya sekondari Nyankumbu Girls Manispaa ya Geita, nakuhudhuriwa na maafisa elimu kutoka mikoa sita, walimu wakuu na wanafunzi huku Mwenyekiti wa maafisa elimu Tanzania Martine Nkwabi amesema lengo la mtihani huo ni kupima uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi, kiwango cha ufundishaji wa walimu, pamoja na kuangalia kama wanafunzi wamepata ujuzi wa kukabiliana na changamoto za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.
Amesema mtihani huo ulihusisha shule 1,401 kati yake shule 1,115 za Serikali na shule binafsi 246 kutoka halmashauri zote 43 pamoja na watahiniwa 151,649, wakiwemo wavulana 74,142 na wasichana 74,424 nakwamba Simiyu imeshika nafasi ya pili kwa asilimia 91.31, nafasi ya tatu ni Shinyanga kwa asilimia 89.71, Kagera nafasi ya nne asilimia 84.35, Geita nafasi ya tano asilimia 83.58 na Mara nafasi ya sita asilimia 80.58.

Miongoni mwa wanafunzi watatu kutoka Geita waliofanya vizuri ni Alex Theojenes James wa Shule ya Sekondari Geita aliyeongoza kwa kupata ufaulu wenye ubora kwa kupata Divisheni 1.7 na Faraja Silas wa shule ya Nyankumbu Girls aliyeibuka nafasi ya tatu kwa upande wa wasichana shule za serikali na kukabidhiwa zawadi na mgeni rasmi.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Dkt Elfas Msenya amesema watahiniwa 6,331 kati yao wavulana wakiwa 3,248 na wasichana 3,083 sawa na asilimia 4,17 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro huku akisisitiza mikoa yote ya kanda ya ziwa kufanya tathmini ya changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati ya kuzitatua haraka kuelekea katika mtihani wa taifa siku chache zijazo.