Storm FM
Storm FM
11 August 2025, 1:49 pm

Mwanamke huyo amekiri kuwa amekuwa akiishi maisha ya mateso kwa kuota ndoto za kutisha akiwa kwenye shughuli hizo za kishirikina.
Na Kale Chongela:
Wakati mikutano ya injili ikiendelea kuwagusa watu katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita, Mwanamke mmoja kutoka nje ya Mkoa wa Geita amewaacha watu midomo wazi baada ya kujitokeza hadharani kwenye umati mkubwa wa watu kwenye mkutano wa Injili na kutangaza kuwa ameachana na uchawi.
Tukio hilo limetokea wakati wa ibada ya jioni katika mkutano wa injili wa siku saba, ambapo mwanamke huyo kwa hiari yake amewakabidhi watumishi wa Mungu vifaa vilivyodaiwa kuwa vya kishirikina kisha viongozi hao wa dini kuviteketeza kwa moto mbele ya mamia ya watu waliojitokeza kwenye mkutano hio.
Mwanamke huyo amekiri kuwa amekuwa akiishi maisha ya mateso kwa kuota ndoto za kutisha ikiwemo za kufanya mauaji kwa muda mrefu nakwamba amechoshwa na hali hiyo na sasa anaanza upya kwa kumkabidhi maisha yake Mungu wa Mbinguni.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakifuatilia mkutano huo kwa karibu wamesema tukio hilo limeonyesha jinsi ambavyo maombi yanaweza kubadilisha maisha ya mtu huku wakiwataka wakazi wa eneo hilo kuendelea kumlilia Mungu ili jamii iendelee kupata wokovu wa kweli.
Viongozi wa kiroho waliopo kwenye mkutano huo walilitazama tukio hilo kama ushahidi wa kazi ya Roho Mtakatifu wakisisitiza kuwa si mwanzo wa maajabu, bali ni mwendelezo wa matendo makuu yanayotokana na huduma ya kiinjili ya mtu kwa mtu.

Mchungaji Eliya George wa Kanisa la TAG “Heri Wenye Moyo Safi”, ambaye alikuwa akihubiri katika mkutano huo, amesema watu wengi wameanza kuokoka na kuukiri wokovu wao kupitia huduma hiyo ya wazi na akatoa wito kwa waumini kuendelea kusali kwa bidii ili waliopotea waokoke.