Storm FM
Storm FM
3 August 2025, 3:40 pm

Klabu ya Yanga imeahidi kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu huu kuliko wakati wowote.
Na Mrisho Sadick:
Klabu ya Soka ya Yanga imeendelea kusherehekea mafanikio yake ya msimu wa 2024/25 kwa kutembeza makombe yake matano katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Geita mkoani Geita Jambo ambalo limevuta hisia za mashabiki wengi waliokuwa na hamasa kubwa kushuhudia mafanikio hayo ya kihistoria.
Msafara huo umeongozwa na msemaji wa klabu hiyo Ali Kamwe na Mkurugenzi wa wanachama, mashabiki na masoko, Ibrahim Samwel ambao wamekuwa kiungo muhimu kati ya klabu hiyo na mashabiki huku msemaji huyo akisema mwaka huu wamejipanga kufanya vizuri michuano ya Kimataifa kutokana na usajili mzuri ambao wameufanya.

Awali akitoa taarifa ya mwenendo wa wanachama katika matawi mratibu wa matawi ya Yanga mkoa wa Geita Rajabu Mohammed amebainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ofisi ya mratibu wa matawi mkoa na usafiri huku mgeni rasmi katika sherehe hizo Hussein Makubi Mwananzara akiahidi kutatua changamoto hizo kwa awamu.

Makombe yaliyotembezwa ni pamoja na Kombe la NBC, Ngao ya Jamii, Muungano Cup, CRDB Cup pamoja na Toyota Cup.