Storm FM
Storm FM
31 July 2025, 8:28 pm

Wafanyabiashara hao wameipongeza benki ya NMB kwa kuwapatia mafunzo juu ya elimu ya fedha na mikopo
Na Mrisho Sadick:
Halmashauri ya Manispaa ya Geita Mkoani Geita imewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanamiliki leseni halali za biashara huku ikisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia kupata ulinzi wa kisheria na kuepuka usumbufu wa mara kwa mara kutoka kwa mamlaka husika.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Biashara wa Manispaa ya Geita Mrisho katika semina ya wafanyabiashara iliyoandaliwa na Benki ya NMB kupitia mpango wake wa NMB Business Club katika ukumbi wa mikutano wa Otonde Plaza mjini Geita.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya biashara wa Benki ya NMB Alex Mgeni amewahamasisha wafanyabiashara hao kuendelea kushirikiana kwa karibu na benki hiyo ili kuiwezesha kuwa na uwezo wa kukopesha makampuni mengi kwa wakati mmoja na kusaidia kukuza uchumi wa ndani huku akisisitiza kuwa Benki hiyo kwasasa ndio Benki pekee nchini yenye mtaji mkubwa na uwezo wa kukopesha fedha nyingi kwa wakati mmoja.

Wafanyabiashara hao akiwemo mwenyekiti wa NMB BUSINESS CLUB Mkoa wa Geita Michael Masusu na Recho Sospiter wameipongeza Benki ya NMB kwa kuwapatia mafunzo juu ya elimu ya fedha na mikopo, ushuru na kodi, bima, masoko, pamoja na taratibu za kupata vibali vya biashara, huku wakihimizwa kuimarisha mahusiano ya kibiashara yatakayochochea maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla.
NMB imesema lengo la mafunzo hayo, mbali na kutoa elimu, ni kuwashukuru wafanyabiashara kwa ushirikiano wao na pia kupata mrejesho wa changamoto wanazokumbana nazo ili kuboresha huduma zake na kuendelea kuwahudumia kwa ufanisi.