Storm FM
Storm FM
24 July 2025, 2:12 pm

Majanga ya moto yameendelea kuwa mwimba mchungu kwa wajasiriamali Geita huku sababu za majanga hayo nyingi zikiwa hazijulikani.
Na Mrisho Sadick:
Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umeteketeza karakana moja ya useremala katika Mtaa wa Nyerere Road Manispaa ya Geita Mkoani Geita nakusababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni tisa.
Kwa mujibu wa mmiliki wa karakana hiyo Adamu Seleman amesema tukio hilo limetokea alfajiri ya Julai 24,2025 baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani kuwa eneo lake la kazi linateketea kwa moto ambapo licha ya Jeshi la zimamoto na uokoaji kufika eneo la tukio moto huo umeteketeza mashine za kisasa, vifaa vya useremala pamoja na bidhaa zilizokuwa zimekamilika tayari kwa ajili ya wateja.
Mmoja wa wafanyakazi kwenye Karakana hiyo Bizideli Kamala amesema Kati ya mali zilizoteketea ni pamoja na vitanda vya mbao, meza, milango, kabati na vyombo mbalimbali vya kazi za useremala ambavyo vilikuwa vikitumika kwa shughuli za kila siku , hasara hiyo kubwa imesababisha sintofahamu na huzuni si kwa wamiliki pekee bali hata kwa wafanyakazi waliokuwa wakitegemea kalakana hiyo kama chanzo chao kikuu cha kipato.

Chanzo halisi cha moto huo bado hakijathibitishwa, huku ikielezwa kuwa huenda ikawa umetokana na hitilafu ya umeme au hujuma nakwamba wataalamu wa zimamoto na mamlaka husika wameanza uchunguzi ili kubaini kiini hasa cha janga hilo ambalo limeacha maumivu kwa familia ya kalakana hiyo pamoja na wateja waliokuwa wakisubiri bidhaa zao huku mashuhuda wa tukio hilo Makoye Masolwa na Mwajabu Omari wakielezea hali ilivyokuwa.

Jeshi la Zimamoto na uokoaji limefika kwa wakati katika eneo la tukio na kufanikiwa kuuzima moto huo kabla haujasambaa kwenye maeneo jirani, hata hivyo hakuna kifaa chochote kilichookolewa katika tukio hilo.