Storm FM

Ajali yaua watumishi wawili wa TRA Geita

21 July 2025, 7:39 pm

Kamanda wa Polisi Geita akizungumzia tukio la ajali. Picha na Mrisho Sadick

Madereva watakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kupumzika ili kuepusha ajali.

Na Mrisho Sadick:

Wafanyakazi wawili wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Mwanza wamefariki Dunia katika ajali mkoani Geita wakati wakitokea Mutukula Mkoani Kagera kutekeleza majukumu yao.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi SACP Safia Jongo amesema ajali hiyo imetokea Julai 20,2025 majira ya saa 10 alfajiri katika eneo la Bwawani mamlaka ya mji mdogo Katoro wilayani Geita.

Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu wawili ambao ni maafisa Forodha Emmanuel Leonard na Mwita John pamoja na majeruhi mmoja Julius Dismas ambaye ni dereva wa gari hilo ambaye alisharuhusiwa kutoka hospitali.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Geita

SACP Jongo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uchovu wa dereva wa gari hiyo ambayo ni mali ya TRA kwakuwa aliendesha gari hilo kwa muda mrefu huku Jeshi la polisi mkoa wa Geita likitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kujipa muda wa kupumzika.