Storm FM
Storm FM
18 July 2025, 7:36 pm

Maandalizi ya uchaguzi mkuu yameendelea kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya mikoa kuendelea kupatiwa mafunzo.
Na Mrisho Sadick:
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka waratibu, wasimamizi na maafisa wa uchaguzi nchini kuhakikisha wanazingatia kiapo walichoapa kwa kujiepusha na vitendo vya uvujishaji wa siri kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria na maadili ya kazi hiyo.
Angalizo hilo limetolewa na Mratibu wa Mafunzo, Mawazo Bikenye kwa niaba ya Mjumbe wa Tume hiyo, Jaji Asina Omari, wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika katika Manispaa ya Geita kuanzia Julai 15 hadi 17, 2025.

Mwenyekiti wa mafunzo hayo Bi Sarah Yohana amesema mafunzo hayo yamewasaidia kwa kiasi kikubwa nakwamba watakwenda kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria , kanuni , taratibu na miongozo na maelekezo mbalimbali kutoka tume huru ya taifa ya uchaguzi.
Mafunzo hayo yalihusisha waratibu wa uchaguzi Mkoa, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi pamoja na maafisa ununuzi kutoka mikoa ya Geita na Kagera, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu.

Washiriki wa mafunzo hayo Damian Alloys kutoka Mkoani Geita na Evodi Kivango kutoka Kagera wameapa kufanya kazi kwa mujibu wa kiapo, huku wakiahidi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi, na kutunza siri za kazi kama ilivyoelekezwa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi.