Storm FM
Storm FM
15 July 2025, 2:01 pm

Jumla ya washiriki 98 kutoka mikoa ya Geita na Kagera wameshiriki katika mafunzo ya siku tatu yaliyoanza leo kuelekea uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Na: Ester Mabula – Geita
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza leo Julai 15 na yanatarajiwa kukamilika Julai 17 mwaka huu na yanafanyika katika ukumbi wa EPZA mjini Geita ambapo jumla ya mada 12 zitatolewa kwa washiriki sambamba na kuwawezesha kubadilishana uzoefu.
Washiriki hao ni pamoja na waratibu wa uchaguzi mkoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi na maafisa ununuzi.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo mgeni rasmi ambaye ni Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa mahakama kuu Asna Omari amewaasa washiriki kuzingatia kanuni ikiwemo kusoma vyema na kuielewa Katiba pamoja na kusoma miongozo mbalimbali inayotolewa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa hatua zote uhusishe vya vyote vya siasa vyenye usajili kamili na pia waepuke kuwa vyanzo vya malalamiko kwenye mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza maratibu wa uchaguzi mkoa wa Geita Herman Matemu ameshukuru uwepo wa mafunzo hayo na kutoa rai kwa wananchi wa Geita kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wanaofaa.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza matarajio yao baada ya mafunzo na namna gani watashiriki katika kufanikisha mchakato wa uchaguzi.
