Storm FM
Storm FM
14 July 2025, 7:35 pm

Benki ya NMB imeendelea kuwa karibu na walimu ili kuwapunguzia baadhi ya changamoto ambazo ziko ndani ya uwezo wa benki hiyo kama mikopo yenye mashariti nafuu.
Na Mrisho Sadick:
Serikali imeahidi kuendeleza ushirikiano na Benki ya NMB kutokana na mchango wake mkubwa katika kuwathamini na kuwaheshimu walimu kwa kutambua nafasi yao muhimu katika jamii.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela wakati wa ufunguzi wa Programu ya Mwalimu Special uliofanyika Julai 14, 2025, mjini Geita Programu ambayo inaratibiwa na Benki ya NMB.

Walimu zaidi ya 300 kutoka wilayani Geita wameungana kushiriki programu hiyo inayolenga kuwajengea uwezo, kuboresha afya, kuwawezesha kiuchumi na kuwaandaa kwa maisha bora kazini na baada ya kustaafu.
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Faraja Mg’ingo, amesema lengo kuu ni kuwatambua walimu kama nguzo ya maendeleo ya taifa kwa kuwapa elimu ya kifedha, mikopo nafuu ya makazi na kuwahamasisha kutumia fursa mbalimbali za benki hiyo.

Walimu waliopata fursa hiyo wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kupanga maisha yao kwa ufanisi zaidi, huku wakifurahishwa na namna ambavyo NMB inawaunga mkono kwa vitendo nakwamba kaulimbiu ya “Umetufunza, tunakutunza”, imeibuka kuwa kielelezo cha namna taasisi binafsi zinavyoweza kushiriki katika maendeleo ya sekta ya elimu kwa kuwajali wale wanaoijenga.