Storm FM

Mama wa kijana aliyeuawa Bukombe aomba haki itendeke

5 July 2025, 5:07 pm

Mama mzazi wa Enock aliyeuawa Bukombe akizungumza na Storm FM Nyumbani kwakwe. Picha na Edga Rwenduru

Matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yameendelea kuleta athari ikiwemo mauaji ya watu ambao wengine huenda wakawa hawana hatia.

Na Mrisho Sadick:

Mama wa kijana Enock Muhangwa (25) aliyeuawa kwa kipigo katika Kijiji cha Uyovu Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita ameliomba Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua wote waliohusika na tukio hilo.

Akiwa Nyumbani kwakwe katika Kata ya Uyovu mama wa Kijana Enock Bi Kulwa Baseki ameiomba serikali kupitia Jeshi la polisi kuwasaka nakuwakamata watu wote waliohusika katika tukio hilo.

Mama mzazi wa Enock aliyeuawa Bukombe akiwa na ndugu zake Nyumbani kwakwe. Picha na Edga Rwenduru

Tukio hilo lilishika kasi baada ya video kusambaa katika mitandao ya kijamii zikionesha kijana huyo akipigwa huku akiwa amefungwa mikono yake miwili na kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la polisi tukio hilo lilitokea Juni 26,2025 baada ya kijana huyo kutuhumiwa kwa wizi wa kompyuta na mashine za kunyolea ambapo kutokana na kushambuliwa huko alifariki Dunia.

Baadhi ya ndugu na majirani wa familia ya Enock wamesikitishwa na tukio hilo kwa madai kuwa kijana huyo hakuwa na tabia za wizi huku mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Sostenes Maendeleo amelaani vikali tukio hilo.

Mama mzazi wa Enock aliyeuawa Bukombe akiwa katika kaburi la mtoto wake.Picha na Edga Rwenduru

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limefanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo, akiwemo Ferdinand Antony Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika na Hussein Ally  Watuhumiwa wengine wanaendelea kutafutwa.

Sauti ya mwandishi wetu Mrisho Sadick ameripoti taarifa hii