Storm FM

Vijana 80 kulinda shamba la miti Silayo Chato

4 July 2025, 1:50 pm

Vijana waliojitokeza kwenye usaili wa kuomba kazi ya ulinzi wa shamba la miti Silayo Chato wakiwa kwenye paredi. Picha na Mrisho Sadick

Kutokana na matukio ya uharibifu wa misitu nyakati za kiangazi TFS imeamua kuongeza nguvu ya ulinzi wa shamba la miti Silayo

Na Mrisho Sadick:

Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Silayo Wilayani Chato Mkoani Geita imetoa fursa ya ulinzi wa Shamba hilo kwa vijana 80 kutoka katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo kwa lengo la kuzuia uvamizi wa watu wanaotaka kuni, mbao, na mkaa pamoja na hatari ya uchomaji moto.

Zaidi ya vijana 127 wamejitokeza kwenye usaili uliofanyika kwa usimamizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chato, ukihusisha maofisa kutoka Jeshi la Polisi, Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji, TAKUKURU pamoja na Jeshi la uhifadhi.

Kamati ya ulinzi na usalama Chato ikiwa katika usaili wa vijana wa kulinda Shamba la miti Silayo Chato. Mrisho Sadick

Mkuu wa polisi wilaya ya Chato Fred Mpandula  amewataka vijana hao kufanya kazi kwa uzalendo kwakuwa serikali imeona iongeze nguvu kazi katika ulinzi wa shamba hilo kwa kutumia vijana wazawa wa eneo hilo huku Mkuu wa Jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya hiyo Ramadhani Maneno na Afisa Uhamiaji mwandamizi Prolimina Tairo wakiwasihi vijana hao kufanya kazi hiyo kwa bidii.

Sauti ya maafisa wa kamati ya ulinzi na usalama Chatio
Vijana waliojitokeza katika ajira ya muda ya kulunda shamba la miti Silayo wakiwa katika hatua ya kwanza ya kupimwa afya. Picha na Mrisho Sadick

Mhifadhi Mwandamizi Juma Mwita Mseti ambae ni mkuu wa Shamba la miti Silayo amesema ajira hizo ni za muda nakwamba hatua hii imechukuliwa kufuatia ongezeko la matukio ya uvamizi kwenye mashamba ya miti hasa kipindi cha kiangazi.

Sauti ya Mhifadhi mkuu shamba la Silayo

Kwa mujibu wa Wakala wa Misitu na Shirika la FAO, Tanzania inapoteza zaidi ya hekta 400,000 za misitu kila mwaka kutokana na uvunaji haramu wa kuni na mkaa, huku asilimia kubwa ya wananchi wakitegemea nishati hiyo kwa matumizi ya kila siku.