Storm FM

102 wajitokeza kuwania ubunge mkoa wa Geita

3 July 2025, 5:39 pm

Katibu wa siasa uenezi na mafunzo wa CCM Mkoa wa Geita akizungumzia zoezi zima la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lililomalizika jana Julai 03,2025. Picha na Mrisho Sadick

Baada ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi za ubunge na udiwani kumalizika sasa joto limehamia kwenye hatua ya uchujaji wagombea.

Na Mrisho Sadick:

Wanachama wa CCM 102 Kutoka Majimbo tisa ya uchaguzi Mkoani Geita wamejitokeza kuchukua nakurejesha fomu katika zoezi lililoanza rasmi Juni 28 na kufikia tamati Julai 2, 2025 huku Chama hicho kikivuna zaidi ya Milioni 58 kutokana na ada ya uchukuaji wa fomu hizo.

Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Geita, Andrew Mnunke akizungumza na waandishi wa Habari katika Ofisi za CCM Mkoa wa Geita leo Julai 03,2025 amesema jumla ya wanachama 102 wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania Ubunge katika majimbo tisa ya mkoa wa Geita, kati yao, wanaume ni 85 na wanawake 17.

Katibu wa siasa uenezi na mafunzo wa CCM Mkoa wa Geita akizungumzia zoezi zima la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lililomalizika jana Julai 03,2025. Picha na Mrisho Sadick

Katika orodha hiyo, Jimbo la Geita mjini limeongoza kwa kuwa na watia nia wengi ambao ni (18), likifuatiwa na Chato kusini ikiwa na watia nia (18), Katoro (13), Mbogwe (14), Busanda (8), Geita Vijijini (8), Bukombe (1), Chato Kaskazini (15) na Nyang’hwale (7) huku Kwa upande wa Viti Maalum kupitia UWT ni wagombea 15 na kundi la vijana likiwakilishwa na wanachama wawili.

Sauti ya Mwenezi mkoa wa Geita

Katika nafasi za Udiwani, jumla ya wagombea 625 wamejitokeza kuwania nafasi za kawaida katika kata 122, wakiwemo wanaume 543 na wanawake 80. Aidha, wagombea wa Viti Maalum kupitia Udiwani ni wakiwa 141mkoa mzima wa Geita.

Kwa mgawanyo wa kata kulingana na majimbo , Jimbo la Bukombe watia nia waliojitokeza ni 74, Chato Kaskazini na Kusini 40, Busanda 65, Katoro 55, Geita Mjini 89, Geita Vijijini 82, Mbogwe 75 na Nyang’hwale 65.

Mnunke ametoa wito kwa watia nia wote kuwa watulivu wakati Chama hicho kikianza Mchakato wa vikao vya uchujaji wagombea kuanzia siku ya kesho Julai 04,2025 huku akiwatahadharisha baadhi ya wagombea kuacha tabia ya kuanza kampeni kabla ya vikao kumaliza kazi yake.