Storm FM
Storm FM
2 July 2025, 11:38 am

Tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan afungue rasmi Daraja la JP Magufuli ili lianze kutumika kuanzia Juni 19, 2025 wananchi wameendelea kupongeza hatua hiyo.
Na Mrisho Sadick:
Wananchi na wakulima wa Mkoa wa Geita wameendelea kuipongeza serikali kwa kuruhusu Daraja la JP Magufuli kutumika bila malipo kwani imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama na muda wa kusafirisha mazao yao tofauti na awali walipokuwa wakitumia vivuko.
Wakazi wa Mkoa wa Geita na maeneo jirani ya Ziwa Victoria wakiwa katika Daraja hilo wameendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukukamilisha ujenzi wa Daraja hilo kwani kwasasa wananufaika zaidi tofauti na hapo awali.

Diwani wa kata ya Bukoli wilayani Geita anaemaliza muda wake Faraji Rajabu Seif na Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamalembo Manispaa ya Geita Seif Rajabu Seif wamesema daraja hilo limekuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo kwani kwasasa wanauza mazao yao kwa bei nzuri kutokana na urahisi wa kuyafikisha Jijini Mwanza.

Daraja hilo linaunganisha Wilaya ya Misungwi kupitia eneo la Kigongo na Wilaya ya Sengerema kupita eneo la Busisi, likiwa na urefu wa kilomita tatu pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 Kwa sasa limekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya shilingi bilioni 716.3.