Storm FM
Storm FM
14 June 2025, 2:35 pm

Waandishi wa habari wa redio za kijamii kanda ya ziwa wameahidi kwenda kuibua na kusimulia mafanikio ya watu wenye ulemavu kama njia ya kuondoa unyanyapaa
Na Mrisho Sadick:
Watu wenye ulemavu nchini bado wanaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo unyanyapaa kuzuiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi kutokana na jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya kuishi na watu wenye ulemavu.
Kutokana na hali hiyo mtandao wa redio za kijamii Tanzania TADIO umewakutanisha waandishi wa habari zaidi ya 20 kutoka radio 10 za kijamii wanachama wa mtandao huo kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kuripoti nakuandaa vipindi kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu ili kubadili mtazamo wa jamii kuhusu watu wenye ulemavu.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza Juni 13 na 14 mwaka huu yanafanyika Jijini Mwanza katika ukumbi wa mikutano wa Gold Crest , akizungumza katika mafunzo hayo mkufunzi Tuma Dandi amesema mkakati huo wa mafunzo kwa waandishi hao nikwenda kubadili mtazamo wa jamii juu ya watu wenye ulemavu kwakuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi na wengine hawana pa kuzisemea.
Sambamba na hayo Dandi amewasisitiza pia waandishi hao kuwa wakati wanaandaa taarifa na vipindi vyao kuhusu watu wenye ulemavu wazingatie nyaraka muhimu ikiwemo sheria, sera , mikataba ya kimataifa , vitabu kuhusu ulemavu , filamu na muziki.
Baadhi ya waandishi walioshiriki katika mafunzo hayo wameahidi kwenda kuibua na kusimulia mafanikio ya watu wenye ulemavu kama njia ya kuvunja unyanyapaa kwakuwa mafanikio hayo ni ushahidi kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo endapo watapewa fursa na mazingira rafiki.
Sambamba na mafunzo hayo kuhusu watu wenye ulemavu, Mhariri mkuu wa TADIO Hilali Ruhundwa na mtaalamu wa tehama Amua Rushita wamewakumbusha waandishi hao juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili ya kazi yao pamoja na matumizi ya takwimu na uchambuzi wa taarifa ili kuwajengea uwezo wa kuelewa tabia na mahitaji ya wasikilizaji wao kwa kutumia data halisi kwani kupitia takwimu, waandishi wanaweza kujifunza jinsi ya kutathmini maudhui yao, kuona aina ya vipindi vinavyopata usikilizwaji mkubwa, na namna wanavyoweza kuboresha vipindi ili kufikia hadhira kubwa zaidi.