Storm FM
Storm FM
12 June 2025, 3:56 pm

Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale imeendelea kupata hati safi kutoka kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG
Na Mrisho Sadick:
Kaimu mkuu wa mkoa wa Geita ambae ni mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa amewataka watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita kuongeza ufanisi katika usimamizi , ufuatiliaji na uwajibikaji wa shughuli mbalimbali za serikali Ili kupunguza au kumaliza kabisa hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG).
Hajat Fatma Mwasa ametoa kauli hiyo kwenye mkutano maalumu wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo la kujadili majibu ya hoja na mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha 2023/2024 huku mkuu wa wilaya hiyo Grace Kingalame akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Akiwa kwenye baraza hilo Mkaguzi mkuu wa nje wa hesabu za serikali Mkoa wa Geita Waziri Shaban amesema halmashauri hiyo imeendelea kuweka rekodi ya kupata hati safi kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka fedha 2019/2020 hadi 2023/2024 huku akiwataka madiwani kuongeza msukumo kwa baadhi ya mambo ambayo wanaona hayaendi sawa sawa.


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Husna Toni ameahidi kufanyia kazi maagizo na mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye baraza hilo huku mwenyekiti wa Halmashauri hiyo John Isack akisisitiza kila mtumishi kuendelea kuwajibika kwa nafasi yake ili kumaliza hoja hizo.