

2 April 2025, 9:42 am
Kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu baadhi ya makada wa CCM wameanza kutafuta nafasi za uongozi kwa nguvu zote huku wakingine wakianza kuvunja utaratibu wa chama.
Na Mrisho Sadick:
Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Geita kimetoa onyo kali kwa wanachama wake wanao wasumbua madiwani na Wabunge waliopo madarakani kwa kuanza kufanya kampeni za kutafuta nafasi hizo kabla ya mchakato huo kutangazwa rasmi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji Cha Nyankanga Kata ya Nyamalimbe wilayani Geita ambapo amesema wale ambao wanakiuka katiba na kanuni za chama hicho kwa kuanza kampeni mapema nakuwasumbua viongozi ambao bado wapo madarakani kwa mujibu wa Sheria hawatavumiliwa.
Kwa upande wake Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Geita Alexandria Katabi amesema mwanachama yoyote atakaegundulika anafanya mchezo huo atashughulikia kwa mujibu wa taratibu za chama hicho ili kuwalinda viongozi ambao bado wanatekeleza majukumu yao.
Hatua hiyo inakuja kufuatia uwepo wa madai ya baadhi ya watu wanaotaka kuwania nafasi za Udiwani na Ubunge katika hilo kuanza kufanya kampeni kimya kimya huku wakiwabeza viongozi ambao bado wako madarakani.