

31 March 2025, 3:01 pm
Vijana wameamua kutumia fursa zilizopo kijiji kwao kupambana na changamoto ya ajira
Na Edga Rwenduru – Geita
Vijana Taasisi ya TK Movement wasiyokuwa na ajira katika kijiji cha Nyanguku Manispaa ya Geita mkoani Geita wameanzisha miradi ya ufugaji wa Mbuzi,kuku pamoja na uuzaji wa mafuta ya Petrol lengo likiwa ni kujikwamua kiuchumi.
Wakizungumza mara baada ya kutembelewa na viongozi wa Taasisi ya TK Movement mkoa wa Geita vijana hao wamesema mpaka sasa wana mbuzi wapatao sita, kuku 12 na kwa siku wanauza lita saba mpaka kumi za mafuta ya Petrol huku malengo ya kikundi hicho yakiwa ni kuajiri vijana wengi zaidi.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho Fitina Mwingereja amesema hatua hiyo itakuwa mkombozi kwa vijana hao kujikwamua kiuchumi huku akiahidi kushirikiana nao katika harakati hizo kwakuwa zitakuwa chachu kwa vijana wengine kujifunza namna ya kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao.
Mratibu wa Taasisi ya TK Movement Manispaa ya Geita Festo Mgema amesema ni wakati sasa wa vijana wengi kugeuza changamoto walizonazo kuwa fursa ya kujiingizia kipato huku Charles Ochai mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Costantine Kanyasu amesema Ofisi hiyo iko tayari kushirikiana na vijana hao kukuza miradi yao.