Storm FM

Kifua kikuu bado tishio mkoani Geita

24 March 2025, 4:52 pm

Ester Paul , mchimbaji mdogo wa madini katika mgodi wa Imaranguzu. Picha na Mrisho Sadick

Ikiwa leo Tanzania na dunia kwa ujumla inaadhimisha siku ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) imeelezwa kuwa kundi la wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu lipo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo kutokana na idadi kubwa ya wachimbaji hao kutokutumia vifaa vya kujilinda na vumbi wakati wa kazi zao.

Na: Mrisho Sadick – Geita

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Afya, maambukizi ya ugonjwa kifua kikuu yanazidi kupungua ambapo kwa mwaka 2015 watu 306 kati ya watu laki moja waligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu lakini kwa mwaka 2023 watu 195 kati ya watu laki moja ndiyo waliobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo ambapo Takwimu hizo zinaonesha ugonjwa huo upungua kwa asilimia 69 kutoka mwaka 2015 hadi 2023.

Storm FM Imetembelea Migodi iliyopo eneo la Imaranguzu lililopo kata ya Lwamgasa, wilayani Geita kutaka kufahamu jinsi gani wachimbaji wadogo wanachukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo ambapo baadhi yao wanajua athari zitokanazo na ugonjwa huo huku wengine wakiwa hawana elimu yoyote juu ya ugonjwa huo.

Sauti ya wachimbaji
Kaimu mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma mkoa wa Geita Dkt. Festo Manyelezi. Picha na Mrisho Sadick

Kaimu mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma mkoa wa Geita Dkt. Festo Manyelezi akizungumza na Storm FM amesema serikali inakiri kuwa wachimbaji wadogo wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu nakwamba wanaendelea kusisitiza kuwa uchunguzi na matibabu ya ugonjwa huo ni bure katika hospitali zote za umma.

Sauti ya kaimu mratibu wa kifua kikuu na Ukoma Geita Dkt. Festo Manyelezi

Kwa upande wake Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma Manispaa ya Geita Mkoani Geita Dkt. Jackline Mfoy amesema watu zaidi ya 8 hufariki Dunia katika kipindi cha miezi mitatu kutokana na ugonjwa wa Kifua kikuu katika eneo hilo.

Mfoy amesema hali ya maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) katika eneo hilo bado ni kubwa na kwamba kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu wamefanikiwa kuibua wagonjwa zaidi ya 160.

Sauti ya mratibu wa kifua kikuu na Ukoma manispaa ya Geita

Amesema mwaka Jana 2024 walikuwa na wagonjwa wa kifua kikuu 879 huku akiwataka wananchi kufika katika sehemu za kutolea huduma za Afya pindi wahisipo dalili za ugonjwa huo ikiwemo , kutokwa na jasho jingi wakati wa usiku ,kukohoa kwa wiki mbili nakuendelea, kukohoa makohozi ya damu na kupungua uzito.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye mzigo mkubwa wa kifua kikuu, ikichangia asilimia 87 ya wagonjwa wote duniani, Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya ya Tanzania, kumekuwa na maendeleo katika kupambana na kifua kikuu nchini, Vifo vinavyotokana na kifua kikuu Vimepungua kutoka vifo 55,000 mwaka 2015 hadi vifo 25,800 mwaka 2022, sawa na punguzo la asilimia 55.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kifua kikuu kwa mwaka huu 2025 inasema “KWA PAMOJA TUNAWEZA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU: AZIMIA, WEKEZA, TIMIZA”

Wachimbaji wadogo wakiendelea na shughuli katika mgodi wa Imaranguzu. Picha na Mrisho Sadick