

5 March 2025, 11:20 am
Licha ya serikali kuendelea kutoa elimu juu ya athari za vitendo vya ukatili hususani kwa watoto, bado baadhi ya wananchi wameendelea kutenda matukio hayo.
Na: Emmanuel Twimanye – Sengerema
Mtoto mwenye umri wa miaka 14 katika mtaa wa Misheni wilayani Sengerema mkoani Mwanza amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kudaiwa kumwagiwa chai ya moto na bibi yake kwa sababu ya kuchelewa kurudi nyumbani.
Akizungumzia tukio hilo mtoto anaedaiwa kufanyiwa ukatili huo amesema kuwa alikwenda sokoni kuuza sambusa za bibi yake na kuchelewa kurudi nyumbani ndipo alipofanyiwa ukatili huo wa kinyama na bibi yake.
Paulina James ambaye ni bibi anayetuhumiwa kufanya ukatili kwa mtoto huyo amekana kufanya kitendo hicho huku akimtishia mtoto huyo kumfukuza nyumbani kwake.
Baadhi ya wananchi wa mtaa huo wameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali kumchukulia hatua kali kisheria bibi huyo ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mission Joseph Protas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuagiza mtoto huyo kupelekwa hospitali ili kupatiwa huduma ya matibabu kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya bibi huyo.