

25 February 2025, 2:57 pm
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Geita, Kamishna mwandamizi wa polisi SACP Safia Jongo Februari 24, 2025 ametoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya matukio mbalimbali.
Na: Ester Mabula – Geita
Jeshi la polisi mkoa wa Geita linawashikilia watu watatu wa familia moja kwa tuhuma ya mauaji ya baba yao mzazi aitwaye Hussein Bundala, mwenye umri wa miaka 103 aliyeuawa akiwa nyumbani kwake Februari 05, 2025 majira ya saa 2 usiku katika Kitongoji cha Ihananilo, Kata ya Nyamtukuza wilaya ya Nyang’hwale kwa kukatwa na kitu chenye makali sehemu za kichwani, usoni na shingoni.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Yombo Hussein Bundala (75) mwanamke, Makame Hussein Bundala (53) mwanaume na Shija Hussein Bundala (50) mwanaume.
Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kiuchunguzi na watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Katika tukio lingine Kamanda Jongo amethibitisha wanafunzi 7 wa shule ya GESECO kufukuzwa kutokana na vurugu iliyotokea hivi karibuni shuleni hapo.