Storm FM

Wanafunzi 30 mbaroni kwa kuzua vurugu Geita

21 February 2025, 9:55 pm

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Geita akizungumzia tukio la wanafunzi kufanya vurugu. Picha na Edga Rwenduru

Jeshi la polisi latumia nguvu kuwatuliza wanafunzi waliozua vurugu katika shule ya sekondari Geita huku wengine wakitiwa mbaroni.

Na Edga Rwenduru:

Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari Geita GESECO kwa tuhuza za kuwashambulia na kuwajeruhi walimu na walinzi wa shule hiyo pamoja nakuharibu mali za shule wakishinikiza kuachiwa mwanafunzi mwenzao aliyekamatwa na uongozi wa shule akiwa na simu ya mkononi kinyume na utaratibu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi ( ACP) Adam Maro amethibitisha kuwashikilia wanafunzi hao kutokana na vurugu zilizotokea usiku wa kuamkia leo februari 21,2025 hizo nakwamba taratibu zingine za kisheria zinaendelea.

Muonekano wa shule ya sekondari Geita baada ya vurugu kutokea. Picha na Edga Rwenduru

Aidha Kamanda Maro ameongeza kuwa wanafunzi wenzake walivyobaini kuwa mwenzao kasimamishwa masomo walianzisha vurugu tena wakidai kuwa mwenzao arejeshwe shuleni kwasababu ameonewa ambapo katika vurugu hizo pia zimesababisha uharibifu wa mali na ndipo jeshi la polisi liliamua kuingilia kati na kufanikiwa kuwashikilia wanafunzi 30 kwaajili ya mahojiano zaidi.

Sauti ya kaimu kamanda wa Polisi Geita

Katika vurugu hizo aliyekuwa mwalimu wa zamu siku hiyo Lukas Ngalabuto alijeruhiwa kwa kupigwa mawe na wanafunzi hao lakini kwasasa afya yake inaendelea vizuri huku vurugu hizo za wanafunzi zimesababisha hasara ya mali ambapo madirisha ya vioo ya Aluminium yapatayo saba yenye thamani ya milioni mbili yameharibiwa.