

17 February 2025, 5:41 pm
Serikali imeendelea kuimarisha na kuboresha huduma za wizara ya fedha ikiwemo kusogeza huduma hizo karibu na wananchi zaidi.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wizara ya fedha imetoa onyo kwa watu na taasisi mbalimbali za fedha zinazotoa mikopo umiza kwa wananchi kuacha mara moja kwani watakao kiuka agizo hilo watachukulia hatua ikiwemo kufutiwa leseni kwa wale waliorasimishwa kufanya kazi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa nchi, ofisi ya Rais mipango na uwekezaji Mhe. Stanslaus Nyongo kwa niaba ya waziri wa fedha Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizindua Jengo la hazina ndogo lililojenga katika Mtaa wa Magogo Kata ya Bombambili Manispaa ya Geita Mkoani Geita.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo lenye miundombinu ya kisasa leo Februari 17, 2025 mshauri elekezi kutoka wakala wa majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Geita Amina Morsad amesema Jengo hilo limejengwa kwa thamani ya zaidi ya shillingi Bilioni 4 na limekamilika kwa asilimia 100 likiwa na Ofisi 14 na kumbi 2.
Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Mhe. Constantine Kanyasu akiwa katika hafla hiyo licha ya kupongeza ujenzi wa ofisi hizo ameiomba serikali kuboresha miundombinu ya Barabara kwa kiwango cha lami kwenda katika Ofisi hizo na Ofisi zingine za serikali zilizopo katika eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita katika uzinduzi wa Jengo hilo amesema serikali ya awamu ya sita imefanya mapinduzi makubwa kwa kujenga majengo ya kisasa Mkoani Geita.
Katika hatua nyingine Naibu waziri Nyongo amesema serikali imeendelea kuimarisha na kuboresha huduma za wizara ya fedha ikiwemo kusogeza huduma hizo karibu na wananchi na kwamba huduma zitakazotolewa katika Ofisi hizo zitakuwa fungamani sawa sawa na ubora wa Jengo.