

10 February 2025, 3:26 pm
Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Februari 08, 2025 mkoani Geita imepelekea changamoto ya kuathiri baadhi ya makazi ya watu.
Na: Kale Chongela – Geita
Nyumba tano za wakazi wa mtaa wa Ibolelo maarufu kwa jina la Mwabasabi kata ya Nyankumbu halmashauri ya manispaa ya Geita zimeathiriwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Februari 08, 2025.
Wakizungumza baadhi ya wakazi wa nyumba zilizoharibiwa na mvua hiyo wamesema wakati mvua inanyesha ghafla waliona maji yakiibuka chini ya ardhi ndipo ukuta wa nyumba ukaaguka chini.
Baadhi ya mashuhuda wameelezea namna tukio hilo lilivyojitokeza huku wakiiomba serikali kuwasaidia kuweza kujinasua katika changamoto hiyo.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mwabasabi Bw. Juma Ramadhani Luge amekiri kutokea kwa uharibifu wa nyumba 5 katika mtaa wake huku akibainisha kuwa changamoto kubwa ni kutokana baadhi ya maeneo katika mtaa wake kukosa mtaro hali inayosababisha maji kukosa mwelekeo na kusababisha kutuama eneo moja kwa muda mrefu.
Licha ya uharibifu huo wa baadhi ya nyumba kubomoka inaelezwa kuwa hakuna madhara yoyote ya kibinadamu yaliyojitokeza.