Storm FM

Kifua kikuu tishio kwa wachimbaji Geita

4 February 2025, 11:44 am

Mtaalamu wa afya akiendelea na uchunguzi kwa wakazi wa Kata ya Lwamgasa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Licha ya serikali kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya kifua kikuu bure lakini bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kupatiwa huduma hiyo.

Na Mrisho Sadick:

Serikali Mkoani Geita imewataka wamiliki wa migodi midogo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu kuwaruhusu wafanyakazi wake kwenda kuchunguzwa ugonjwa wa kifua kikuu kwakuwa kundi hilo linaongoza kwa maambukizi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Chato Luis Peter kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela kwenye uzinduzi wa kampeni ya Mpango harakishi wa kuwaibua wahisiwa wa ugonjwa huo hususani kwenye migodi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu iliyofanyika katika Kata ya Lwamgasa wilayani Geita.

Amesema takwimu zilizotolewa na shirika la Afya duniani WHO 2024 duniani kote kulikuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu milioni  10.8 na wagonjwa milioni 1.2 walifariki dunia nakwamba kwa Tanzania katika mwaka huo kulikuwa na wagonjwa 120,000 sawa na wagonjwa 183 kwa kila wagonjwa 100,000 huku kwa mkoa wa Geita wagonjwa walioibuliwa katika kipindi hicho ni 88 ikiwa ni idadi ndogo ya malengo yaliyokusudiwa.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Chato
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni ya mpango wa uibuaji wahisiwa wa kifua kikuu. Picha na Mrisho Sadick

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoani Geita Michael Mashala amesema wametoa elimu kwa zaidi ya watu 1,000 kati yao 802 wamefanyiwa uchunguzi na 267 wamehisiwa kuwa na ugonjwa huo nakwamba kundi la wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Mkoani Geita liko katika hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo, amewasisitiza wamiliki wa migodi midogo ya uchimbaji wa madini kuwaruhusu wachimbaji hao kwenda kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huo wakati wa zoezi zima la upimaji wakati wa kampeni hiyo.

Sauti ya Mratibu wa Kifua kikuu na ukoma

Baadhi ya wachimbaji wa madini katika kata ya Lwamgasa wameipongeza serikali kufikisha huduma hiyo karibu na wananchi nakwamba walikuwa wanashindwa kufuata huduma hizo katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita kutokana gharama za kufika katika eneo.

Muonekano katika picha shughuli za uchimbaji wa madini ya dhabau Lwamgasa Geita . Picha na Mrisho Sadick