

4 February 2025, 9:47 am
Matukio ya mifugo aina ya ng’ombe kuibiwa na kuchinjwa nyakati za usiku yameendelea kuacha maswali kwa wananchi katika mitaa mbalimbali ya manispaa ya Geita.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wakazi wa mtaa wa Elimu kata ya Nyankumbu halmashauri ya manispaa ya Geita wamelalamikia kukithiri kwa matukio ya wizi wa mifugo aina ya ng’ombe ambapo mifugo hiyo inakutwa imechinjwa na wezi na kuondoka na nyama huku wakiiomba serikali kuchukua hatua za haraka ili kunusuru mifugo yao.
Wakizungumza na Storm FM wakazi wa eneo hilo wamesema matukio hayo yamezidi kuongezeka huku wakiliomba jeshi la polisi kuwasaidia kwani licha ya jitihada zinazofanywa na polisi jamii wa mtaa huo bado watuhumiwa wamekuwa wakirejea mtaani na kuendelea kufanya uhalifu.
Mwenyekiti wa mtaa wa Elimu Hassan Mshole amesema tayari wameanza mikakati ya kuhakikisha wanapambana na matukio hayo ya wizi kwa kuitisha mikutano ya hadhara na kupiga kura ili kutambua ni watu gani wanaotekeleza matukio hayo huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pindi wanapoitajika kwaajili ya kutoa ushahidi.
Diwani wa kata ya Nyankumbu John Mapesa ameliomba Jeshi la polisi kufuatilia matukio hayo kwani inaonekana vijana wanaotekeleza matukio hayo ya kuchinja mifugo ya watu na kuondoka na nyama wanapata oda kutoka kwenye migahawa na huuza nyama hiyo kwa bei nafuu ikilinganishwa na zile za buchani.
Storm FM inafanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Geita ili kuweza kufahamu mikakati zaidi katika kukomesha matukio haya.