

3 February 2025, 5:12 pm
Kilele cha wiki ya sheria nchini hufanyika kwa kujumuisha shughuli mbalimbali zinazohusiana na masuala ya sheria ili kuelimisha wananchi na kuhamasisha matumizi bora ya sheria katika jamii.
Na: Ester Mabula – Geita
Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Geita Kelvin Mhina amesema mashauri zaidi ya elfu nane sawa na asimilia 94.2 yamesikilizwa na kukamilishwa kwa mwaka 2024 ikiwa ni miongoni mwa malengo waliyojiwekea ya kumaliza kesi zote kwa wakati na kwa viwango vya juu zaidi.
Jaji Mhina ameyasema hayo leo februari 03, 2025 katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan zamani EPZA mkoani Geita ambapo amesema matumizi ya TEHAMA katika shughuli za mahakama yamesaidia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo kwani ndio ukuaji wa teknlojia.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amesema serikali itaendelea kuboresha mifumo zaidi ili kurahisisha shughuli za kimahakama sambamba na kuweza kuwasaidia watanzania juu ya masuala mbalimbali kuhusu haki.
Katika hatua nyingine RC Shigela amewataka waandishi wa habari kuandika habari za kesi za madai kwa uwazi bila kuogopa usalama wao kwani atahakikisha analinda usalama wao
Kauli mbiu mbiu katika maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini ni “TANZANIA YA 2050: NAFASI YA TAASISI ZINAZOSIMAMIA HAKI MADAI KATIKA KUFIKIA MALENGO MAKUU YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO“