Wananchi Mpomvu washiriki ujenzi wa kituo cha Afya
13 January 2025, 5:39 pm
Baada ya kuwepo kwa changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika maeneo jirani, hatimaye kata ya Mtakuja yaanza ujenzi wa kituo cha Afya.
Na: Kale Chongela – Geita
Wananchi wa mtaa wa Mpomvu kata ya Mtakuja manispaa ya Geita wameungana kwa pamoja kushiriki zoezi la kuchimba msingi katika ujenzi wa kituo cha afya mpomvu.
Wananchi hao wakiwa eneo la ujenzi wa kituo hicho cha afya Januari 09, 2025 wameiambia Storm FM kuwa hapo awali walikuwa wakienda kupata huduma kituo cha afya cha Nyankumbu kwani Mpomvu ilikuwa na zahanati hali ambayo ilikuwa ikiwalazimu kutumia gharama za usafiri hadi kufika Nyankumbu.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mpomvu Bw. Charles Manyanga ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa jitihada hizo za kujenga kituo cha afya Mpomvu kwani itasaidia kuondoa changamoto ya wananchi wa eneo hilo.
Kaimu mganga mfawidhi wa zahanati ya Mpomvu Dkt. Ayoub Daudi amesema kukamilika kwa ujenzi huo itasaidia kuongeza kiwango kikubwa cha utoaji wa huduma kwa hadhi ya kituo cha afya na kwamba tayari wameshapokea milioni mia tano awamu ya kwanza katika ujenzi huo.