Mume adaiwa kumuua mke wake Katoro
10 January 2025, 12:53 pm
Migogoro ya kifamilia imeendelea kutajwa kuwa chanzo cha anguko la familia ambapo hupelekea changamoto mbalimbali ikiwemo ongezeko la vitendo vya ukatili miongoni mwa wanandoa.
Na: Daniel Magwina – Geita
Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Adventina Nicholaus mwenye umri wa miaka 37 mkazi wa kata ya Ludete katika mamlaka ya mji mdogo wa Katoro mkoani Geita adaiwa kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na mume wake eneo la nyonga katika mwili wake huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa kuwa mgogoro wa kifamilia.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Januari 07, 2025 nyumbani kwake mtaa wa Ludete mamlaka ya mji mdogo wa Katoro ambapo baadhi ya ndugu wa marehemu wamesema mwanaume huyo baada ya kutekeleza tukio hilo alitokomea kusiko julikana kisha kuanza kuwapigia simu ndugu wa marehemu juu ya tukio hilo akiomba msamaha.
Ally Mataru ni miongoni mwa wananchi waliohudhuria na kushiriki katika mazishi ambapo amelaani tukio hilo na kuishauri jamii kuacha kujichukulia sheria mkoani wanapokumbana na migogoro ya kifamilia.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Katoro Dkt. Yohana Kitutu amethibitisha kumpokea mwanamke huyo akiwa amefariki kutoka kituo cha afya binafsi cha Lisabon alikokuwa amepelekwa baada ya kufanyiwa ukatili huo.